NIDA Kusitisha Matumizi Ya NIN (Namba Ya NIDA) Kwa Wasiochukuwa Vitambulisho

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, ametangaza kuwa kuanzia tarehe 1 Mei, 2025, matumizi ya Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) kwa baadhi ya wananchi yatafungwa rasmi hadi pale wahusika watakapojitokeza kuchukua vitambulisho vyao.

Kaji ametoa taarifa hiyo Aprili 14, 2025 wakati akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, jijini Dar es Salaam. Amesema hatua hiyo inalenga kuhimiza uwajibikaji miongoni mwa wananchi waliokwisha tumiwa taarifa na kushindwa kujitokeza bila sababu za msingi kuchukua vitambulisho vyao.

“Kwa kuzingatia kuwa tulishatuma sms kwa watu karibu wote ambao vitambulisho vyao vilikusanywa na kuwaarifu wajitokeze kuvichukua, sasa tunawajulisha rasmi kuwa matumizi ya NIN kwa watu hao yatasitishwa hadi watakapojitokeza kuchukua vitambulisho vyao,” alisema Kaji.

Vile vile amewahimiza wananchi kufika katika ofisi za NIDA kuchukua vitambulisho vyao ili kuepuka usumbufu wowote wa kupata huduma zinazohitaji uthibitisho wa utambulisho.

Aidha, Kaji alifafanua kuwa tangu kuanza kwa zoezi la kukusanya vitambulisho na kutuma sms mwezi Januari 2025 hadi kufikia Machi 23, 2025, jumla ya wananchi 1,880,608 sawa na asilimia 157 ya idadi ya watu ambao hawajachukua vitambulisho walitumiwa ujumbe.

“Wakati tunavikusanya vitambulisho hivyo kutoka ofisi za Kata, Vijiji na Mitaa, tulikuwa na vitambulisho 1,200,000 vilivyokuwa havijachukuliwa. Hii inaonyesha kuwa takribani kila aliyekuwa hajachukua kitambulisho chake ameshapokea ujumbe,” Aliongeza Kaji.

Kati ya ujumbe huo, sms 680,608 zilitumwa kwa waombaji wapya waliosajiliwa katika kipindi hicho na ambao vitambulisho vyao tayari vimechapishwa na kusubiri kuchukuliwa.

NIDA inasisitiza kuwa kuchukua kitambulisho cha Taifa ni wajibu wa kila raia, kwani kitambulisho ni msingi wa kupata huduma muhimu kama vile benki, mawasiliano, ajira, elimu, afya na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.

Makala Nyingine:

kujisajili NIDA online (Kitambulisho Cha Taifa)